FOR SALE: Wenger kuwauza Ozil na SanchezKila chenye mwanzo, kina mwisho. Ndicho unachoweza kusema baada ya Kocha Arsene Wenger kufunguka  zama za Mesut Ozil na Alexis Sanchez kuendelea kuwa wachezaji wa Arsenal zimefika mwisho.

Kwa mara ya kwanza, Wenger amenyanyua kinywa chake na kufikiria kumpiga bei Ozil Januari kama hatasaini mkataba mpya sasa.

Wakala wa Ozil, amesema mteja wake yupo kwenye mazungumzo na mambo yanaendelea vizuri hasa kutokana na matakwa yake ya kutaka kubaki England, lakini Kocha Wenger amesema kitu tofauti, akidai hakuna makubaliano yaliyofikiwa na kama itakuwa hivyo hadi Januari, basi watakachofanya ni kumuuza tu.

Wenger hataki kumpoteza bure staa huyo aliyemsajili kwa ada ya Pauni 42.5 milioni kama atamuacha hadi mwishoni mwa msimu, hivyo anataka kumuuza tu Januari. Mchakato huo unaweza kumhusu pia Sanchez, ambaye pia mkataba wake unafika kikomo mwisho wa msimu na bado hajasaini dili jipya.

Wenger alipoulizwa kama Ozil atauzwa Januari, alisema: “Tutafikiria kila uwezekano, kuna nafasi kubwa ya kumuuza Januari. Sijaweka kikomo cha lini haya mambo ya mkataba mpya yanaweza kusainiwa, lakini tunataka hilo limemalizwe kwa haraka.”

Kama Ozil na Sanchez hawatakuwa wamesaini mikataba mipya watakuwa na ruhusu ya kuzungumza na klabu nyingine inayohitaji huduma zao itakapofika Januari na wanaweza pia kusaini mikataba ya awali ya klabu hizo.

Wakala wa Ozil, Erkut Sogut juzi alikutana na Wenger kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kiungo huyo kuhusiana na hatima yake ndani ya timu hiyo na mambo sasa yanaonekana kocha huyo wa Arsenal amechoka na anachofikiria ni kumpiga bei tu.

Inter Milan imeonyesha nia ya kumtaka Ozil, lakini Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho naye anampigia hesabu kiungo huyo aliyewahi kufanya naye kazi Real Madrid.

Wenger hataki kuuza silaha hizo kwa wapinzani wake ndani ya Ligi Kuu England, lakini Ozil mpango wake ni kubaki Arsenal hadi mwisho wa mkataba wake kwani hapo atakuwa huru kwenda kujiunga na timu anayoitaka.

Sanchez bado hajarejea kuungana na wenzake kikosi cha Arsenal.

No comments

Theme images by lobaaaato. Powered by Blogger.