Bilioni 2.2 Serikali yatenga kupunguza madeni ya wakandarasi

Serikali kupitia Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamad Masauni imesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Jeshi la Polisi limetenga jumla ya shilingi Bilion 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya Wakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali ya Jeshi hilo.


Mh. Masauni ameyasema hayo, bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jaku Ayoub kuhusu madai ya Mkandarasi aliyejenga vituo vya Polisi Mkokotoni Unguja na Madungu.

Mhandisi Masauni ameeleza kuwa fedha hizo zilizotengwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni ambao umetengewa jumla ya shilingi Milioni 200 ikiwa ni sehemu anayodai mkandarasi huyo.

“Serikali inatambua madeni ya Wakandarasi wote ikiwemo Albatna Builing Contractor na ina nia ya dhati ya kuyalipa madeni yote ya Wakandarasi na washauri elekezi waliohusika katika miradi mbalimbali ikiwemo miradi iliyohusisha Jeshi la Polisi,” amefafanua Masauni.
Wakati huohuo Masauni amesema kuwa, Serikali imekuwa na mpango wa kupeleka fedha za Maendeleo kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa samani katika Magereza nchini ikiwemo Gereza la Karanga.

“Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatekeleza mpango wa muda mrefu wa kuyaboresha majengo hayo kwa kuyafanyia ukarabati mkubwa unaolenga kuyaimarisha, kuyaboresha na kuyafanyia upanuzi,” amengeza Masauni.
Aidha amesema kuwa, kutokana na ufinyu wa bajeti fedha hizo zimekuwa zikitolewa kwa awamu katika Magereza mbalimbali nchini ili kufanikisha uboreshaji wa majengo hayo.

No comments

Theme images by lobaaaato. Powered by Blogger.