Wasanii waahidi kukinukisha kesho, Fiesta 2017 Leaders ClubMsimu wa shamrashamra za muziki na utamaduni katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wa tamasha la Tigo Fiesta 2017, wenye kaulimbiu ya ‘Tumekusoma’, unatarajiwa kuhitimishwa kesho kwenye viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, ukihusisha wasanii zaidi ya 18.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, alisema kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 16 ya tamasha hilo, Tigo Fiesta ilikuwa imewashirikisha wasanii wa Kitanzania pekee.

“Kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2017 kitawahusisha wasanii wa Kitanzania pekee. Tigo imejikita kuleta mageuzi makubwa kwa kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa na ajira kwa vijana nchini. Tumewakutanisha wasanii wetu maarufu na mashabiki wao katika mikoa yote 16 tuliyotembelea na kuwajengea uwezo wa kutumbuiza laivu mbele ya halaiki kubwa ya watu,” alisema Mpinga.

Alisema kuwa kupitia Tigo Fiesta 2017, wameibua vipaji vya muziki katika mikoa mbalimbali kupitia shindano la kuimba la Supa Nyota, ambapo washindi watapata fursa ya kutumbuiza katika kilele cha msimu kesho.

Alisema wameamua kutumia wasanii wa ndani, kwani wameona wana uwezo wa kukata kiu ya muziki ya Watanzania bila hata kuwa na msanii kutoka nje ya nchi.

Mpinga alisema kuwa, katika matamasha ya mikoani, wasanii hao wamethibitisha kuwa wanaweza kuwaburudisha mashabiki wao, kwani walifanya mambo makubwa, huku pia mwitikio wa mashabiki ukiwa ni mkubwa, kwa kuwa wengi walijitokeza kushuhudia burudani kutoka kwa wasanii wao.

“Kununua tiketi ni rahisi. Fuata utaratibu wa kawaida wa kutuma pesa na tuma Sh 9,000 kwenda namba ya Tigopesa 0678 888 888. Hapo hapo utapokea ujumbe mfupi wa SMS unaothibitisha manunuzi yako ya tiketi. Hifadhi huo ujumbe mfupi. Baadaye utapokea maelekezo ya jinsi na wapi pa kwenda kuchukua tiketi yako. Bei halisi ya tiketi getini ni Sh 10,000,” alisema Mpinga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandilizi ya Tigo Fiesta 2017, Sebastian Maganga, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi Leaders Club akiwaahidi kupata burudani ya hali ya juu, huku pia akiwahakikishia ulinzi wa kutosha, hasa wakati wa kutoka.

“Tamasha la Tigo Fiesta litaanza mapema tu, milango itafunguliwa saa sita mchana na kutakuwa na matukio mbalimbali yanayolingana na muda huo na itakapofika saa moja jioni, moto utawashwa rasmi kwa wasanii kuanza kulishambulia jukwaa kama nyuki hadi saa saba usiku,” alisema Maganga.

Maganga aliwataja wasanii watakaotoa burudani kesho katika tamasha hilo kuwa ni Ali Kiba, Aslay, Ben Pol, Barnaba, Chege, Darasa, Dogo Janja, Jux, Fid-Q, Rostam (Roma na Stamina), Rich Mavoko na Nandy.

Wengine ni Mr Blue, Vanessa Mdee, Maua Sama, Zaiid, Lulu Diva, Mimi Mars, Rosa Ree, Chin Beez, Nyandu Tozi, Nedy Music, Ommy Dimpoz, Bright, Weusi (Joh Makini, G-Nako na Nikki wa Pili) na wengineo.

Alisema kuwa, tamasha hilo kwa mwaka huu limezunguka katika mikoa ya Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mbeya, Moshi na Mtwara.

Wakizungumzia maandalizi yao, wasanii watakaopanda jukwaani kesho wameahidi kutowaangusha wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake watakaofika Leaders kesho.

Ben Pol akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema kuwa, wamejipanga vilivyo kufanya mambo makubwa kesho, kila mmoja wao akiwa amepanga kufanya ‘surprise’ ya aina yake itakayoifanya siku hiyo kuwa ya kukumbukwa.

“Wapenzi wa burudani waje kwa wingi Leaders kushuhudia tukihitimisha msimu huu wa Tigo Fiesta kwa weledi wa aina yake, kila mmoja wetu amejiandaa vya kutosha kufanya shoo ‘bab kubwa’, karibuni sana,” alisema.

Naye Vanessa Mdee, alisema: “Wakazi wa Dar es Salaam watarajie shoo kabambe zaidi ya ilivyokuwa mikoani, kwa upande wetu wasanii tumejipanga kufanya shoo kali, hatutawaangusha hata kidogo.”

Pamoja na wasanii hao kuahidi kufanya mambo makubwa, wakazi wa Dar es Salaam bila shaka watakuwa na hamu ya kuona mkali wa Bongo Fleva, Ali Kiba anayetamba na wimbo wake wa Seduce Me anafanya nini kesho baada ya kufunika kwenye matamasha ya mikoani.

Vilevile, dogo anayesumbua kwa sasa, Aslay, ambaye ameonekana kuwateka wapenzi wa muziki nchini baada ya kutoa nyimbo mpya 13 ndani ya muda mfupi, naye anasubiriwa kwa hamu kuona iwapo atapagawisha kama alivyofanya mikoani.

Akitamba na nyimbo zake mpya za Pusha, Natamba, Mario, Danga, Rudi, Kidawa na nyinginezo, Aslay anatajwa kuwa msanii aliyeongoza kwa kupewa ushirikiano wa hali ya juu na mashabiki wakati wote wa tamasha la Tigo Fiesta ambapo mashabiki walikuwa wakiimba naye na kucheza nyimbo zake kwa hisia kali.

Katika majukwaa yote aliyopanda jukwaani, idadi kubwa ya watu waliohudhuria shoo za tamasha hilo, waliimba pamoja na Aslay na mwisho wa siku, kumshangilia vilivyo kijana huyo aliyemeguka kutoka Bendi ya Yamoto.

Aslay alisema kuwa, amejipanga vilivyo kuhakikisha anafanya shoo ya nguvu jijini Dar es Salaam kesho, kama ilivyo kawaida yake.

“Jumamosi pale Leaders Club, Dar es Salaam ndio kilele cha Tigo Fiesta, nimejipanga kufanya mambo makubwa, hivyo wapenzi wa muziki na burudani wajitokeze kwa wingi siku hiyo sitawaangusha hata kidogo,” anasema.

No comments

Theme images by lobaaaato. Powered by Blogger.