Kiki za mastaa hawa zilitikisa Nigeria 2017 (+Uchambuzi)Na: Omary Ramsey

Zimebaki siku 11 pekee kabla ya kuuaga mwaka 2017 na mengi yametokea kwa kipindi chote cha miezi 12 iliyopita, hasa kwenye tasnia ya burudani.

Mitandao ya kijamii imekuwa ikipambwa na habari mbalimbali za wanamuziki, waigizaji wa filamu na hata watangazaji maarufu wa vipindi vya televisheni na redio.

Hawa ni baadhi tu ya mastaa waliokuwa gumzo kutokana na mafanikio au matukio yao ya nje ya kazi zao, yaani ‘kiki’ kama inavyofahamika na wengi.


Wizkid


Kwa mwaka mzima jina la mwimbaji huyo lilikuwa halikosi kwenye vyanzo vya habari. Ngoma yake ya ‘One Dance’ aliyomshirikisha rapa Drake ndiyo iliyoongoza kwa kutazamwa zaidi (watu bilioni 1.1) na kuingia kwenye kitabu cha Guinness World Record.

Lakini pia, singo yake ya pili iitwayo ‘Come Closer’ aliyompa tena shavu Drake iliweza kuwa gumzo si       tu Nigeria, bali Afrika kwa ujumla.

Tukio jingine lililomfanya staa huyo kuendelea kung’ara ni lile la kumaliza tiketi kabla ya siku ya ‘show’ yake ya jijini London iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Royal Albert Hall.

Hakuishia hapo, kwani Novemba 2017 akanyakua tuzo tatu kwenye tuzo za AFRIMMA zilizofanyika Lagos. Pia, baadaye akatajwa kuwa mshindi wa kipengele cha Msanii Bora wa Kimataifa kwenye tuzo za MOBO.

Mafanikio hayo yalimfanya Wizkid kupokea ujumbe wa pongezi kutoka kwa Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari.

Davido


Staa huyo kuwa gumzo kulitokana na ngoma zake‘IF’, ‘Fall’ na ‘Fia’ ambazo zilitokea kupendwa na kuwavutia mashabiki wengi. Akashinda tuzo mbili za MTV EMA na kisha kubeba moja kwenye zile za MOBO.

Ukiacha bifu lake na Wizkid, pia kitendo cha kupata mtoto wa pili kilimpa ‘kiki’kwenye mazungumzo ya kila siku ya mashabiki wa muziki.

Banky W


Si tu kwenye soko la muziki, pia Banky W alikuwa na mambo mengi nje ya sanaa hiyo yaliyomfanya kuzungumziwa sana.

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana aliachia filamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la ‘The Wedding Party’ ambayo imeendelea kufanya vizuri hadi sasa.

Mbali na hiyo, tukio lake jingine lililompaisha mwaka huu na kumfanya kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii, ni lile la kutangaza kufunga ndoa na mrembo Adesua Etomi. ‘Funika bovu’ ni pale walipofunga ndoa ya kifahari jijini Lagos na kisha kwenda Cape Town, Afrika Kusini.

Tiwa Savage


Ingeshangaza kuiona orodha ya waliozungumziwa zaidi mwaka 2017 bila jina la mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 37. Kwanza, alisainiwa na lebo ya Roc Nation inayomilikiwa na rapa wa Marekani, Jay-Z.

Nje ya muziki, penzi lake na Tee Billz lilikuwa habari ya mjini, hasa baada ya mwanaume huyo kumfuata jukwaani na kumtandika busu.

Ngoma zake ‘All Over’ na ‘Ma Lo’ nazo hazikubaki nyuma katika kumfanya Tiwa azungumzie kwenye mitandao ya kijamii.

Tekno


Mbali na singo zake kubamba vilivyo kwenye soko la muziki la Nigeria, kuna matukio mawili yaliyomng’arisha zaidi.

Kwanza, mshikaji huyo alisaini mkataba mnono wa matangazo na kampuni ya Ciroc ambayo inajishughulisha na uuzaji wa pombe kali. P. Diddy ni miongoni mwa mastaa wanaotumika kuinadi kampuni hiyo.

Tukio la pili lililomfanya Tekno kuzungumziwa zaidi mwaka huu, ni lile la kuweka wazi uhusiano wake wa kimapenzi na mwimbaji Lola Rae.

P Square


Kundi la mapacha Peter na Paul nalo lilizungumziwa zaidi kwa mwaka huu, hasa baada ya taarifa za kuvunjika kwake.

Kuvunjika kwa kundi hilo hakujatokea ghafla tu, ilikuwa ni baada ya taarifa za wawili hao kutoelewana, ambazo zilichukua takribani miezi minne.

Moja kati ya matukio yaliyowafanya wawili hao wazungumziwe zaidi kwenye mitandao ya kijamii, ni video iliyosambaa ikiwaonesha wakitaka kutwangana.

Baada ya kutengana, bado waliendelea kutupiana maneno na hivi karibuni Paul mwenyewe aliwaambia mashabiki wa muziki kuwa wasisubiri kuona P Square likirejea.


Tonto Dikeh


Huyo ni mwigizaji mwenye jina kubwa kwenye soko la filamu la Nigeria ‘Nollywood’.

Mwaka 2017 unamalizika akiwa mmoja kati ya mastaa waliozungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii, hasa kwa matukio yake ya nje ya sanaa.

Kubwa zaidi ni vita yake na aliyekuwa mumewe, Oladunni Churchill. Kutokana na maneno makali ambayo walikuwa wakitupiana kila uchwao baada ya kuvunjika kwa ndoa yao, wawili hao walipamba vichwa vya habari si tu kwenye magazeti, bali hata kwenye mitandao ya kijamii.


Mr. Eazi


Ukiacha kazi zake hasa ‘mixtape’aliyoipachika jina la ‘Life Is Eazi, Vol. 1 – Accra To Lagos’, mapenzi yamempa kiki jamaa huyo kwa mwaka huu wa 2017.

Taarifa za kutoka na Temi Otedola, binti wa bilione Femi Otedola, zilimfanya kila shabiki wa burudani Nigeria atake kumjua Mr. Eazi.

Lakini pia, alikuwa gumzo zaidi alipowajia juu wanamuziki wa Nigeria akiwaambia waache kuiga sauti za wenzao wa Ghana.

No comments

Theme images by lobaaaato. Powered by Blogger.