Orodha ya makocha wanaolipwa kibosi EnglandNa: Omary Ramsey

5. Antonio Conte – Chelsea 


Pauni 125,000 kwa wiki
Baada ya kuifikisha Italia robo fainali ya Euro 2016; huku akiwa amefanya vizuri pia kwenye kikosi cha Juventus ambacho kilibeba ubingwa wa Serie A kwa misimu mitatu mfululizo kati ya 2011 na 2014, Antonio Conte akaonekana anafaa kuinoa Chelsea na katika msimu wake wa kwanza tu aliisaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. 

Kocha huyo baada ya kubeba ubingwa tu, aliripotiwa kupewa ofa ya kuongeza mkataba zaidi, ambapo ripoti zinadai aliitolea nje ofa hiyo. Mshahara wa Muitaliano huyo kwa wiki ni Pauni 125,000 kwa wiki huko Stamford Bridge. 

4. Jurgen Klopp – Liverpool 


Pauni 135,000 kwa wiki 
Jurgen Klopp amelifanya jina lake kuwa maarufu baada ya kufanya kazi kubwa akiwa na Borussia Dortmund, wakati alipobeba ubingwa wa Bundesliga kwa misimu miwili mfululizo 2010/2011 na 2011/2012. 

Mjerumani huyo aliifikisha Dortmund fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pia katika msimu wa 2012/2013. Kwa sasa huduma yake anaitoa Liverpool baada ya kunaswa mwaka 2015. Kibarua cha Anfield kinamfanya Klopp kuwa mmoja kati ya makocha wanaolipwa vizuri tu kwenye Ligi Kuu England kutokana na kuweka kibindoni Pauni 135,000 kwa wiki. 


3. Arsene Wenger – Arsenal 


Pauni 160,000 kwa wiki 
Usishangae kwanini Arsene Wenger huwa anasuasua sana katika kukubali kuwalipa mishahara mikubwa wachezaji wake anaogopa watamfunika. 

Mesut Ozil na Alexis Sanchez alimchemsha kocha huyo kwa kutaka walipwe Pauni 300,000 kwa wiki, jambo ambalo Wenger analiona ni gumu ukizingatia mshahara wake wa wiki ni Pauni 160,000. 

Hata hivyo, pesa hiyo inamfanya Wenger kuwa miongoni mwa makocha wanaolipwa vizuri kwenye Ligi Kuu England akiwa kocha namba tatu nyuma ya Jose Mourinho na Pep Guardiola. 

2. Pep Guardiola – Man City 


Pauni 388,000 kwa wiki 
Anasifa zote kwanza za kuwa mchezaji mahiri kabisa enzi zake kabla ya kuja kuwa kocha matata katika kizazi hiki cha kisasa. 

Pep Guardiola amelifanya jina lake kuwa na hadhi kubwa kwenye soka baada ya kufanya vizuri kweli alipokuwa Barcelona ambapo alibeba mataji 14 katika kipindi cha miaka minne tu aliyokuwapo hapo. 

Alienda Bayern Munich akatamba kabla ya sasa kukimbiza huko England akiwa kwenye kikosi cha Manchester City. 

Mhispaniola huyo ni mmoja kati ya makocha wanaolipwa mishahara mizuri England, akipokea Pauni 388,000 kwa wiki. 

1. Jose Mourinho – Man United 


Pauni 388,000 kwa wiki 
Mmoja kati ya makocha wenye mafanikio makubwa kwenye ulimwengu wa soka na hakika jina lake ni maarufu kwelikweli. Jose Mourinho amefanya kazi Ureno, Italia, Hispania na sasa England akifanya hivyo mara ya pili. 

Katika msimu wake wa kwanza klabuni Manchester United mambo hayakuwa mazuri sana baada ya kumaliza ligi kwenye nafasi ya sita, lakini akiisaidia timu hiyo kurudi Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushinda ubingwa wa Europa League. 

Mshahara wa Mourinho si wa kitoto, kwa wiki anapokea Pauni 388,000 kwa huduma yake Old Trafford.

No comments

Theme images by lobaaaato. Powered by Blogger.